Monday , 4th Apr , 2022

Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hussein Bashe amesema kuwa kwa kipindi ambacho amekuwa bungeni, Rais Samia ndiye Rais pekee aliyeipatia nafasi sekta ya kilimo katika hotuba yake.

Mhe. Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo

Bashe ametoa kauli hiyo leo Aprili 4, 2022 alipokuwa akizungumza katika hafla ya kukabidhi pikipiki kwa maafisa ugani kilimo ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha wanapata vitendea kazi ili kukuza sekta ya kilimo.

"Lakini Mhe. Rais na mimi nataka niseme bila unafiki, kabisa. Nimekuwa mbunge tangu 2015, nimesikiliza hotuba tatu za Marais, wewe ni Rais pekee uliyeipatia nafasi sekta ya kilimo" - Husseinbashe, Waziri wa Kilimo 

Katika hatua nyingine, Waziri Bashe ametoa takwimu ya hali ya mafuta ya kula nchini ambapo amesema mahitaji ya Tanzania ni wastani wa tani laki sita na nusu kwa mwaka huku uzalishaji wa ndani ukiwa hauzidi laki mbili na arobaini kwa mwaka.

Kwa upande wake Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Innocent Bashungwa, amesema hatavumilia kuona maafisa ugani wakishindwa kuwafikia wakulima kwa sababu ya kukosa mafuta kwa ajili ya pikipiki.

"Nitoe wito kwa wakurugenzi, nisisikie kwamba afisa ugani ameshindwa kuwafikia wakulima kisa kakosa mafuta"- Innocent Bashungwa, Waziri OR-TAMISEMI