Wednesday , 24th Dec , 2014

Umoja wa katiba ya wananchi Ukawa umelitaka Bunge lijalo liiwajibishe serikali kwa kutotekeleza kikamilifu maazimio yake kuhusu watuhumiwa katika sakata la Escrow

Umoja wa katiba ya wananchi Ukawa umelitaka Bunge lijalo liiwajibishe serikali kwa kutotekeleza kikamilifu maazimio ya bunge huku wakitishia kuandamana nchi nzima endapo waliohusishwa na tuhuma za ufisadi wa Escrow hawatachukuliwa hatua za kisheria.

Vyama hivyo vimesema havijaridhishwa na mwenendo wa hatua zinazochukuliwa na serikali za kuwawajibisha viongozi waliohusika na uchotwaji wa fedha katika sakata la Tegeta Escrow.

Wakiongea leo jijini Dar es salaam wenyeviti kutoka chama cha Wananchi CUF Prof.Ibrahim Lipumba pamoja na Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Dkt. Wilbroad Slaa wamesema endapo viongozi waliohusika na kashfa hiyo hawatachukuliwa hatua Bunge lijalo liiwajibishe serikali kwa kutotekeleza maazimio ya Bunge.

Prof Ibrahim Lipumba amesema sheria ya maadili inatakiwa itungwe upya na utaratibu wa viongozi kutangaza mali zao uwe wa wazi kwa wananchi na kuongeza kuwa maandamano hayo yana lengo la kulaani ufisadi wa Escrow pamoja na kushinikiza utekelezaji wa maazimio yote ya bunge.

Kwa upande wake katibu mkuu wa Chadema Dk Willbroad Silaa akizungumza katika kikao hicho amesema kuwajibika peke yake haitoshi badala yake hatua za kisheria zinatakiwa zichukuliwe ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo vimeonekana kujirudia mara kwa mara kutokana na watu kutenda makosa na kuishia kujiuzulu ilihali kuna hasara ambazo taifa limeingia.

Kwa Upande Wake Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi Mhe. James Mbatia amesema hotuba wa Rais imezishafisha kampuni za IPTL na PAP huku ilikandamiza shirika la Umeme nchini TANESCO

Mbatia ni miongoni mwa viongozi wa Ukawa walioshiriki kikao hicho ambapo ametumia fursa hiyo kuwasihi viongozi wa dini na viongozi wastaafu waliotumikia taifa kutumia siku kuu ya Noel kupaza sauti zao katika kuhakikisha serikali inasimamia haki na kwamba taifa lolote lenye migogoro haliwezi kupata ustawi wa jamii.