Umoja wa Katiba ya wananchi UKAWA katika mkoa wa Kigoma umewataka watanzania kuchukua hatua dhidi ya Chama cha mapinduzi kutokana na kushindwa kuisimamia serikali na kusababisha wizi, kupanda kwa gharama za maisha na wananchi kushindwa kumudu mahitaji ya msingi kutokana na ubinafsi wa viongozi.
Akihutubia mkutano wa hadhara mbunge wa Kigoma Kusini kupitia chama cha NCCR Mageuzi ambaye pia ni mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa ya NCCR Mh. David Kafulila amesema ili kuiondoa CCM madarakani inahitaji umoja wa wapinzani na wananchi ambao kwa muda mrefu wanateseka na maisha magumu huku watu wachache wakijinufaisha na mali za serikali.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na maendeleo mkoa wa Kigoma Ali Kisala, amevitaka vyama vyote vya upinzani mkoani humo kuunganisha nguvu ili kuiondoa CCM madarakani.