Tuesday , 3rd Aug , 2021

'Sports Countdown' ya EA redio inakupitisha kwenye zile stori kali za sita zilizochukua uzito wa juu kwenye viwanja mbali mbali vya michezo kila siku ya Jumatatu hadi Ijumaa saa moja na robo asubuhi kupitia shoo ya Breakfast ya EA Radio.

Luka Doncic wa klabu ya Dallas Mavericks inayoshiriki NBA nchini Marekani na timu ya taifa ya Slovenia.

6 – Ni idadi ya mabao aliyofunga kiungo mshambuliaji wa klabu ya Aston Villa, Jack Grealish kwenye msimu uliopita pamoja na assist 12 hivyo kuhusika kwenye mabao 18 kiwango ambacho kinawatoa udenda matajiri wa Manchester, klabuya Manchester City ambao wanaelezwa kuwa kwenye mazungumzo ya kutaka kumnasa mkali huyo wa kudemka na mpira kwa paundi mil100.

Licha ya mazungumzo ya usajili wake kwenda vizuri, Grealish ameripoti kambini na kuanza mazoezi na timu yake ya Aston Villa huku ripoti zikieleza kuwa mpaka kufikia mwanzo wa wiki ijayo kuna uwezekano mkubwa dili likakamilika na nyota huyo akajiunga na Mabingwa hao watetezi wa EPL na kuwaongezea makali kwenye safu ya ushambuliaji inayoongozwa na KBD.

5 – Ni idadi ya mabao yaliyofungwa siku ya Jana kwenye michezo mitatu ya michuano ya CECAFA KAGAME CUP, Express ya Uganda iliifunga Atlabara ya Sudan Kusini 1-0 kutoka kundi A wakati kutoka kundi B, Le Messager Ngozi ya Burundi ilitoka sare ya 1-1 na KMKM ya visiwani Zanzibar wakati bingwa mtetezi, KCCA ya Uganda ikinyukwa 2-0 na Azam FC.

Michuano hiyo inataraji kuendelea tena siku ya keshi kutwa Agosti 5 kwa michezo miwili kutoka kundi A, ambapo Nyasa Big Bullet ya Malawi itacheza na Express ya Uganda saa 7 mchana huku Yanga kupepetuana na Atlabara ya Sudan Kusini saa 10 kamili jioni.

4 – Ni idadi ya timu zilizofanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali kwa upande wa soka kwenye michuano ya Olympic inayoendelea jijini Tokyo nchini Japan, timu hizo ni mwenyeji wa michunao hiyo, timu ya taifa ya Japan ambayo imepangwa kucheza na Spain saa 5:00 asubuhi  wakati mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Brazil itacheza na Mexico saa 8:00 za mchana.

3 – Ni idadi ya watanzania wanariadha waliopo nchini Japan kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Olympic, wafukuza upepo hao ni Faulina Abdi ambaye atakimbi amarathon ya wanawake Jumamosi ya saa 1 asubuhi ya Agosti 7.

Wengine ni Alphonce Simbu na Gabriel Gaey ambao watakimbia saa 1 asubuhi ya Jumapili Agosti 8 mwaka huu.

2 – Ni idadi ya nafasi anazoweza kuzicheza mlinzi wa klabu ya Juventus na timu ya taifa ya Italy, Mkongwe Giorgio Chiellini ambaye usiku wa kuamkia leo amegubikwa na furaha baada ya klabu yake ya Juventus kumuongezea kandarasi ya miaka 2 kuendelea kusalia klabu hapo hadi Julai 2023 ambapo atakuwa anatimiza umri wa miaka 38 na miaka 18 ya kuitumikia klabu hiyo.

Ikumbukwe Chiellini kwasasa ana umri wa miaka 36 na ni miongoni mwa wachezaji wenye historia kubwa na klabu ya Juventus tokea kuwemo kwenye kikosi cha kuipandisha daraja na kuirdisha timu ligi kuu mwaka 2007 baada ya kushushwa daraja kwa kashfa ya upangaji matokeo lakini tokea hapo amebeba mataji 14 katika miaka 16 aliyoitumikia timu hiyo.

1 - Ni nafasi anayoshikilia nyota wa Dallas Mvaericks, Luka Doncic kwa kuwa mchezaji maarufu zaidi kwenye kikosi cha timu yake ya taifa ya Slovenia kutokana na ubora anaouoneshwa kwenye ligi ya bora ya kikapu duniani, NBA ya nchini Marekani.

Taarifa zinaeleza kuwa nyota huyo atasaini kandarasi ya miaka 5 kuendelea kuitumikia klabu yake ya Dallas Mavericks hadi mwaka 2026 kwa mkataba wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 202 sawa na bilioni 468 na zaidi ya milioni 419 za kitanzania.