Monday , 2nd Aug , 2021

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro RC Martini Shigella amesema hatua inayofuata mara baada ya kudhibiti moto uliotokea katika kituo cha kupoza umeme Msamvu cha Shirika la Umeme Tanzania TANESCO, ni kuanza uchunguzi wa kubaini chanza cha moto huo.

Picha shughuli zakuzima moto zikiendelea katika kituo cha kupoza umeme cha Msamvu.

RC Shigela amefika katika kituo hiko cha kupoza umeme, na kupongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha wanadhibiti moto huo ambao unamaafa makubwa kwa mkoa wa Morogoro.

“Hatua itakayofuata tutaunda kamati maalum itakayohusisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama pamoja na TANESCO kuhakikisha tunaanza uchunguzi kubaini chanzo cha moto huu, hatua ya pili ni kuhakikisha tunarudisha upatikanaji wa umeme katika mkoa wetu najua chanzo hiki hakiwezi kuleta umeme hivyo wataangalia wapi wanachukulia umeme kwa haraka,” amesema RC Shigela

Akizungumzia madhara ya moto huo RC Shigela amesema “Kama mnavyoona hili jengo ambalo limeungua hapa ni jengo ambalo lina-control na kuruhusu umeme utoke katika substation hii kubwa ambao inalisha 50%, 60% ya mkoa wa Morogoro kuungua kwa substation kumeleta madhara makubwa kwa uendeshaji na matumizi ya umeme na shughuli zote za uzalishaji katika mkoa wetu”.