Thursday , 8th Jul , 2021

Klabu ya PSG ya Ufaransa imetangaza kukamilisha usajili wa beki wa kimataifa wa Hispania Sergio Ramos mwenye umri wa miaka 35 kwa mkataba wa miaka miwili mpaka mwaka 2023. Anajiunga na matajiri hao wa Paris akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na Real Madrid mwezi Juni.

Sergio Ramos

Usajili wa Ramos unakuwa usajili wa tatu (3) PSG wanakamilisha kwenye dirisha hili kubwa la usajili la majira ya joto, wachezaji wengine ambao wameshasajiliwa mpaka sasa ni Achraf Hakimi raia wa Morocco ambaye amejiunga akitokea Inter Milan ya Italia kwa ada ya uhamisho ya Euro million 60 ambayo ni zaidi ya billion 164 kwa pesa za kitanzania na mchezaji mwingine ni kiungo wa kimataifa wa Uholanzi Georginio Wijnaldum ambaye amejiunga akitokea Liverpool akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba.

Ramos anajiunga na PSG baada ya miaka 16 ya utumishi ndani ya kikosi cha Real Madrid ambapo alijiunga na mabingwa hao wa kihistoria wa ulaya mwaka 2005 akitokea Sevilla.

Jumla ameshinda mataji 22 akiwa na Los Blancos ukiwemo ubingwa wa Ligi Kuu Hispania La Liga mara tano (5) na ubingwa wa klabu bingwa ulaya mara nne (4) lakini pia Ramos ni mshindi wa kombe la Dunia mwaka 2010 akiwa na timu ya taifa ya Hispania na ubingwa wa mataifa barani ulaya Euro mara mbili mwaka 2008 na 2012.

Sergio Ramos amesaini mkataba wa Miaka 2 na PSG

Ameondoka Madrid baada ya kumaliza mkataba na hawakufikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya baada ya kutofikia makubaliano ya baadhi ya vipengele ikiwemo muda wa mkataba ambapo mchezaji alikuwa anataka miaka miwili lakini klabu ilikuwa imeandaa mkataba wa mwaka mmoja, ingawa Ramos alinukuliwa akisema kuwa ilifika wakati alikubali kusaini mkataba huo lakini akaambiwa mkataba huo haupo tena.

Anategemewa kuongeza ubora na uzoefu kwenye safu ya ulinzi ya PSG kwa mabeki wa kati ambayo inaundwa na Presnel Kimpembe na Marquinhos.