Jorginho (katikati) akishangilia huku akiwa anapongezwa na wachezaji wenzake wa timu ya taifa ya Itali, Matteo Pessina (kushoto) na Domenico Berardi (kulia) baada ya Jorginho kufunga penalti ya mwisho na ya ushindi kupeleka Italy fainali ya UEFA EUROS 2020.
Bao la Itali liliwekwa kimiani na winga wake hatari, Federico Chiesa dakika ya 60 na mshambuliaji wa Hispania, Alvaro Morata akaisawazishia timu yake dakika ya 80 akipokea pasi ya usaidizi kutoka kwa kiungo Dani Olmo nakufanya miamba hiyo kutoshana nguvu ndani ya dakika 90.
Baada ya sare hiyo, zilizongezwa dakika 30 ili kumsaka mwana fainali mmoja na hatimaye wakalazimika kwenda kwenye changamoto ya mikwaju ya penalti baada ya matokeo ya sare kusalia ndani ya dakika 120 za jumla.
Itali ilikuwa ya kwanza kupiga penalti kupitia kwa kiungo wake Manuel Locatelli aliyekosa pamoja na Dani Olmo wa Hispania. Andrea Belotti, Leonardo Bonucci na Federico Bernadeschi walifunga kwa upande wa Itali.
Kwa upande Hispania, Gerard Moreno, Thiago Alcantara ndiyo wachezaji pekee waliofunga wakati Alvaro Morata alikosa penalti ya 4 na kufanya matokeo kuwa na faida ya mabao 3 ya penalti kwa Itali ilhali 2 kwa Hispania.
Penalti ya mwisho na ya ushindi ilifungwa na kiungo, Jorginho aliyempeleka mlinda mlango Unai Simon upande tofauti na uelekeo wa mpira nakuwafanya Itali kutinga fainali hiyo kwa mara ya kwanza tokea mwaka 2012 ilhali wanatinga fainali kwa mara yao ya nne kwenye michuano hiyo.
Italia pia wameendelea na rekodi ya kutokufungwa tokea Septemba 2018 hadi leo, kwani wamecheza michezo 33 bila kufungwa hata mchezo mmoja kwenye michuano yote na kubakisha ushindi kwenye michezo mitatu ili kuipiku rekodi ya Brazil yakucheza michezo 35 bila kufungwa.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Itali, Roberto Mancini amesema anayo furaha sana ya kuwaburudisha waitaliano wote licha ya kwamba wanamchezo wa fainali umesalia huku akikiri kuwavulia kofia Hispania kwa kuonesha soka safi na upinzani mkubwa sana.
Wakati mabingwa hao wa EURO wa mwaka 1968 wakisheherekea kutinga fainali, kwa upande wa mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, Hispania kupitia kocha wake Luis Enrique amesema siyo siku mbaya kwake kwasababu hayo ni matokeo ya soka.
Enrique amesema wametolewa lakini ameridhishwa na kiwango cha timu na kuondoka kwenye michuano hiyo kama miongoni mwa timu bora ukizingatia alisema mwanzoni kuwa wao ni timu ya nane kupewa nafasi ya kutwaa ubingwa lakini wanaona ni fahari kuonesha shindani mkubwa sana.
Sasa Itali itacheza fainali na mshindi wa mchezo wa England dhidi ya Dernmark mchezo utakaochezwa saa 4:00 usiku wa leo kwenye dimba la Wembley nchini England.



