Thursday , 27th Nov , 2014

SHIRIKA la hifadhi za Taifa (TANAPA) jana limezindua vivutio vipya viwili vya utalii, ikiwemo njia ya kutembea kwa miguu (board walk way) katika eneo la Maji moto ndani ya hifadhi ya Ziwa Manyara, kwa lengo la kuwavutia watalii wengi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu.

Akizungumza katika uzinduzi huo ,Waziri Nyalandu amesema ya kuwa Wizara yake imejipanga kuhakikisha inatimiza malengo yake ya muda mfupi na muda mrefu ya kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni tano kwa mwaka .

Nyalandu amesema wanafanya kila linalowezekana kuongeza idadi ya watalii milioni tano, kwa mwaka na lengo hilo wameligawa katika awamu mbili za muda mfupi wamelenga kupata watalii milioni mbili na muda mrefu watalii milioni tano.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Allan Kijazi, amesema sababu za kuanzishwa kwa miradi hiyo, kuwa inalengo la kuongeza wigo mpana wa watalii, kujionea kwa karibu namna wanyama kama viboko, nyati wanavyopishana Ziwani pamoja na ndege aina kwa aina.

Amesema huduma hiyo ni tofauti sana na itavutia sana watalii na wameboresha vivutio vyetu, katika maeneo haya ya hatari kwa maisha ya watalii waweze kuwaona kwa karibu wanyama na ndege ,lakini pia eneo ndipo yalipo maji ya moto yanapoingia ziwani kitu kinachovutia sana kutizama, waweze kuangalia bila kuhatarisha maisha yao.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Ardhi Maliasili na Mazingira James Lembeli Wakuu wa Mikoa ya Arusha na Manyara,mbunge wa Mbulu Mustafa Akonaay , wadau mbalimbali wa utalii toka serikalini na sekta binafsi pamoja na wananchi.