Wednesday , 28th Apr , 2021

Mabingwa wa kihistoria ya michuano ya klabu bingwa barani Ulaya, Klabu ya Real Madrid imelazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Chelsea kwenye uwanja wake wa nyumbani kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya michuano hiyo usiku wa kuamkia leo.

Mshambuliaji wa Chelsea, Christian Pulisic akimtoka mlinda mlango wa Real Madrid ambapo alifanikiwa na kufunga bao la kwanza la Chelsea.

Chelsea ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa winga wake, Christian Pulisic dakika ya 14 kabla ya mshambuliaji wa Real Madrid, Karim Benzema kushawazisha dakika 15 baadae na kufanya mchezo huokuisha kwa sare na Chelsea kuwa na faida ya bao la ugenini.

Baada ya mchezo huo kumalizika ambao ulikuwa ni wa 450 kwa Madrid kwenye michuano ya Ulaya, Kocha wa timu hiyo, Zinedine Zidane amesema kiujumla wamefurahishwa na matokeo hayo na kusisitiza bado wapo mchezoni kwani wanaimani watapata ushindi nchini England.

Zidane amesema, “Tulivyopata bao, tulikuwa vizuri na tulimiliki mchezo zaidi. Tupo mchezoni na tunaenda kwenye mchezo wa mkondo wa pili na dhamira ya kupata ushindi. Kiujumla, tunafuraha na matokeo haya ya usiku wa leo”.

Kwa upande wa kocha wa Chelsea, Thomas Tuchel amesema hajapendezwa na matokeo hayo kwani kikosi chake kingeweza kupata zaidi ya bao hilo moja ambalo lingewafanya waumalize mchezo huo kabisa.

“Haikuwa bahati wakapata bao kupitia mpira wa kutengwa, lakini hawakuwa na hatari nyingine zaidi, hatuwaruhusu kutengenza nafasi kabisa. Sikufurahishwa na matokeo hayo kwenye ungwe ya kwanza na la muhimu ni kwamba tulibaki kuwa watulivu na hatukupoteza hali ya kujiamini”.

“Kipindi cha pili kilikuwa cha mbinu sana, na unaweza kuona tulikuwa tumechokakwa kiasi Fulani. Tulikuwa na siku chache za kupumzika baada ya mchezo uliopita wa ugenini. Imetubidi tuondoke na sare ya 1-1”.

Bao alilofunga Pulisic limemfanya aweke rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Chelsea mwenye umri mdogo, miaka 22 na siku 221 kufunga bao kwenye hatua ya nusu fainali pamoja na kuwa Mmarekani mwenye mabao mengi kwenye michuano hiyo, mabao matano.

Kwa upande wa Benzema, amemfikisha mabao 71 na kushika nafasi ya nne  sawa na Raul Gonzalez kenye orodha ya wafungaji wenye mabao mengi wa muda wote kwenye historia ya michuano hiyo akizidiwa na Cristiano Ronaldo, Lionel Messi na Robert Lewandowski.

Vile vile amekuwa mfungaji mwenye umri mkubwa wa Real Madrid kwenye historia ya mochuano hiyo akiwa na umri wa miaka 33 na siku 129 tokea Cristiano Ronaldo alipofunga bao alipokuwa na miaka 32 na siku 86.

Sare ya mabao kuanzia mawili au ushindi wowote utaivusha Real Madrid fainali ilhali Chelsea wanahitaji sare ya bila kufungana au ushindi wowote kufika fainali wawili hao watakaporudiana tarehe 5 mei 2021 kwenye uwanja wa Chelsea, Stamford Bridge nchini England.