Tuesday , 22nd Sep , 2020

Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na maendeleo,(CHADEMA) ametaja sababu ya watu kuwa maskini ni pamoja na kuporomoshwa kwa msingi mkuu wa kiuchumi.

Mgombea urais kupitia CHADEMA Tundu Lissu akiwa katika picha ya pamoja na Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dk. Benson Bagonza alipkuwa huko kwaajili ya kampeni.

Amesema hayo wakati anazungumza na wakazi wa Karagwe mkoani Kagera leo Septemba 22, ambapo amesema zao la kahawa limeleta neema ingawa kwasasa  bei ya kahawa imeanguka kutoka shilingi  2100 hadi 1100.

 "Bei ya kahawa imeanguka kutoka sh 2,100 mpaka leo ni shilingi 1,100, watu wamekuwa maskini kwa sababu zao lao kuu la biashara na msingi wao mkuu wa kiuchumi umeporomoka "alisema Tundu Lissu

Aidha Lissu amesema kuwa serikali ya chadema kwa kulitambua hilo endapo itapata madaraka itaifanya mikoa ya mipakani kuwa maeneo maalum ya uchumi na biashara.

“Mikoa ya mipakani tutaifanya kuwa maeneo maalum ya uchumi na biashara maana yake wakulima wa Karagwe kama bei kubwa ipo Uganda serikali itakuruhusu kuuza kahawa yako Uganda " alisema Tundu Lissu

Katika hatua nyingine Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dk. Benson Bagonza amewataka wananchi wakaragwe kufanya maamuzi ya busara katika kuchagua wagombea watakao wawakilisha vyema ikiwa ni pamoja na kushughulikia kero zao.