Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, mh. Lazaro Nyalandu.
Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, mheshimiwa Lazaro Nyalandu, leo amezindua Mamlaka ya Wanyamapori ijulikanayo kama TAWA, itakayokuwa na jukumu la kusimamia ulinzi na uendelezaji wa rasilimali za misitu na wanyamapori nchini.
Kutangazwa kwa mamlaka hiyo kunaenda sambamba na kuzinduliwa kwa mwongozo wa usimamizi wa rasilimali za misitu na wanyamapori, mwongozo unaozikutanisha pamoja wizara na idara za serikali zenye jukumu la ulinzi wa maliasili za misitu na mazingira.
Aidha, waziri Nyalandu amesema mbali ya mwongozo huo, wizara yake kwa kushirikiana na wizara nyingine za mambo ya ndani ya nchi, wizara ya sheria na katiba pamoja na wizara ya uchukuzi, imeanzisha kikosi kazi maalumu kitakachojishughulisha na kuzuia uhalifu wa kimataifa ukiwemo ujangili na usafirishaji wa dawa za kulevya.
Aidha, waziri Nyalandu amesema kuwa hivi karibu kutakuwa na kongamano la kimataifa kuhusu uhifadhi litakalofanyika jijini Arusha ambalo pamoja na mambo mengine, litaangalia namna nchi za Tanzania, Kenya na Mozambique zitakavyoshirikiana kudhibiti ujangili.
Amesema yeye kama waziri wa maliasili na utalii atakutana na wenzake kutoka nchi zaidi ya tisa zilizoalikwa kushiriki kongamano hilo, kujadili namna ya kukabiliana na ujangili unaofanywa na majangili kutoka nje ya mipaka ya nchi husika.