Tuesday , 28th Oct , 2014

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Hanoi asubuhi ya jana, Jumatatu, Oktoba 27, 2014 kuanza ziara rasmi ya siku mbili ya Kiserikali nchini Vietnam.

Rais Kikwete amewasili mjini Hanoi akitokea nchi jirani ya Jamhuri ya Watu wa China ambako Jumapili, Oktoba 26, 2014 alimaliza ziara rasmi ya Kiserikali yeye mafaniko makubwa ya siku sita nchini humo.

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Noi Bai mjini Hanoi, Rais Kikwete amepokelewa na viongozi wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam na baada ya mapumziko mafupi, Rais Kikwete amekwenda Kasri ya Kirais kukutana na Rais Truong Tan Sang kwa mazungumzo ya faragha na baadaye kwa mazungumzo ya Serikali kati ya Tanzania na Vietnam.

Mara baada ya kuwasili kwenye Kasri hiyo, Rais alipokelewa na Rais Sang na akakagua gwaride la heshima ambalo liliundwa na Jeshi la nchi hiyo lililokuwa na vikosi vya anga, maji na nchi kavu.

Baada ya mazungumzo hayo, Marais hao wawili wameshuhudia utiaji saini wa Makubaliano katika Usafiri wa Majini (Marine Transport) ambao umetiwa saini na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe kwa niaba ya Tanzania na Waziri wa Usafirishaji wa Vietnam, Mheshimiwa Dinh Li Thang kwa niaba ya nchi yake.

Mbali na kukutana na Rais Sang, Rais Kikwete baadaye amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam, Mheshimiwa Nguyen Phu Trong, ambaye pia ndiye kiongozi mkuu wa nchi hiyo. Viongozi hao wawili wamekutana kwenye Makao Makuu ya Kamati Kuu ya Chama hicho cha Kikomunisti, yanayoangaliana na Kasri ya Rais.

Rais Kikwete pia amefanya ziara kwenye Makao Makuu ya Kampuni ya Simu ya Viettel ambayo inajiandaa kuingia katika soko la vijijini katika Tanzania. Wakati wa mazungumzo kati ya Rais Kikwete na viongozi wa Kampuni hiyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Juliet Kairuki ameukabidhi uongozi wa Kampuni hiyo hati ya kuanzishwa kwa Kituo hicho.

Baadaye usiku, Rais Kikwete amehudhuria Hafla ya Chakula cha Jioni iliyoandaliwa kwa heshima yake na mwenyeji wake Rais Sang kwenye Kituo cha Kimataifa cha International Convention Centre mjini Hanoi. Rais Kikwete ataendelea na ziara yake ya Vietnam leo kwa kutembelea sehemu mbali mbali na kukutana na Spika wa Bunge la Vietnam, Mheshimiwa Nguyen Sinh Hung.

Hiyo ni ziara ya kwanza kufanywa na Mheshimiwa Kikwete akiwa Rais wa Tanzania, lakini hiyo ni mara ya pili kwake kutembelea Vietnam. Alitembelea Vietnam mwaka 2004, akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.