Monday , 17th Aug , 2020

Watumishi wa Umma wametakiwa kufuata maadili na miongozo iliyopo Kikatiba pindi wanapotoa huduma kwa wananchi ili kupusha migongano ya kimaslahi ambayo hupelekea migogoro katika maeneo ya kazi.

Jaji Mstaafu Harold Nsekela Kamishna wa Maadili, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma.

Hayo yameelezwa na Kamishna wa Maadili, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma, Jaji Mstaafu Harold Nsekela wakati akifungua mafunzo kwa wafanyakazi wa tume ya maadili ambao watakuwa ndio wawasilisha mada katika vyombo vya habari ili kutoa elimu kwa wananchi ipasavyo.

Amesema kuwa lengo la mafunzo hayo      ni kuongeza uelewa namna ya kuepuka mgongano wa maslahi katika utumishi pamoja na kuimarisha njia na mbinu za uwasilishaji mada kwa vyombo vya habari.

“Unaweza ongea kitu kwa nia nzuri ila namna unavyoliwasilisha kwa Umma likaleta madhara hasi, kwahiyo kupitia mafunzo haya mtaelekezwa namna ya kuwasiliana”, amesema Jaji Nsekela.

Ameongeza kuwa” Ilani ya Chama tawala 2015 imeagiza na imeandika kuhusiana na hili suala la kuepuka migongano ya maslahi hivyo linapaswa kutekelezwa kwa vitendo”.

Mafunzo hayo kwa wafanyakazi wa tume ya maadili yatafanyika kwa siku tano lengo likiwa ni kuwajengea uwezo kabla ya kuwapatia mafunzo viongozi wa Umma.