
Winga wa Inter Mila, Alexis Sanchez akiwa kwenye majukum ya kuitumikia klabu yake.
Raia huyo wa Chile mwenye umri wa miaka 31 amesaini mkataba wa miaka mitatu wa kuichezea Nerazurri ambapo pia amekubali kupunguzwa kwa mshahara wake kutoka paundi laki nne kwa wiki hadi laki moja na nusu.
Akiwa na Inter amecheza michezo 29 na kuifungia mabao manne kwenye mashindano yote,ingawa tangu ajiungea na Man United mwaka 2018 alicheza mechi 45 na kufunga mabao matano tu kabla ya kutimkia Italia kwa mkopo.
Huo unakua usajili wa tatu kwa Inter kutwaa wachezaji kutoka Man United akiwemo Romelu Lukaku na Ashley Young.
JE NI FAIDA KWA INTER NA SANCHEZ?
Klabu ya Inter Milan imeanza kurejesha makali yake katika soka la Ulaya,ambapo msimu ujao itashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hivyo inahitaji wachezaji wenye uzoefu na mashindano hayo,akiwemo Alexis Sanchez.
Ikumbukwe Sanchez alianza kuonyesha makali yake akiwa na klabu ya Udinese ya Italia, baadae alijiunga na Barcelona ya Hispania mwaka 2011,ambapo alicheza jumla ya michezo 141 na kufunga mabao 47 pia aliisaidia kutwaa taji la La Liga, copa Del Rey ,Supa Copa de espana, Uefa Super Cup na Klabu Bingwa ya Dunia.
Baada ya mafanikio hayo alitimkia nchini Uingereza katika klabu ya Arsenal mwaka 2014, na kuibuka kuwa miongoni mwa wachezaji muhimu wa kikosi cha The Gunners na kuisaidia timu hiyo kushinda mataji ya FA Cup na Ngao ya Jamii.
Alijiunga na Man United mwaka 2018, ambapo hakupata nafasi kubwa ya kucheza lakini bado anadhihirisha ni mchezaji wa mataji ikizingatiwa akiwa na Timu yake ya Taifa walibeba kombe la Mataifa ya America Kusini.
Uwepo wake ndani ya Inter kumewasaidia kumaliza kwenye nafasi ya pili katika Serie A kwa mara ya kwanza baada ya miaka 9, hivyo huenda akawa chachu ya ushindi wa Inter msimu ujao.