
Watia nia wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CHADEMA, Tundu Lissu na Lazaro Nyalandu.
Jumla ya watia nia saba ndiyo waliorejesha fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo ndani ya CHADEMA, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, mwingine ni aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, Wakili Simba Neo, Leonard Manyama, Gasper Mwanalelya, Lazaro Nyalandu na Dk. Mayrose Majinge.
Wagombea wa nafasi hiyo Bara na Zanzibar watajulikana baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kuanza kujifungia toka jana kupitia na kujadili majina ya wagombea waliotia nia katika nafasi hiyo, ambapo jana kamati hiyo ilianza vikao vyake vya mchujo ambavyo vinafanyika kwa siku tatu mfululizo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene, Kamati Kuu ilianza kutafiti majina ya wagombea hao jana, na leo watapigiwa kura na baadaye yatawasilisha kwa Baraza Kuu la chama hicho ambalo linaketi leo.
Makene amesema baada ya Baraza Kuu kupitisha majina ya wagombea hao kwa Jamhuri na Zanzibar, yatakabidhiwa kwa Katibu Mkuu wa chama hicho leo ambaye naye atayawasilisha katika Mkutano Mkuu utakaofanyikia kesho kwa ajili ya uamuzi wa mwisho.