Sunday , 19th Jul , 2020

Jeshi la Polisi Nchini limesema kuwa linaendelea kuimarisha hali ya usalama na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.

Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime

Taarifa hiyo imetolewa  hii leo na Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime, ambapo amesema kuwa kwa sasa hali ni shwari  japokuwa hivi karibuni kumekuwa na matukio ya kuungua moto kwa Shule mbili ambazo ni Ilala na Kinondoni Islamic zilizosababisha vifo vya wanafunzi watatu.

Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini vyanzo vya moto huo na kuwataka wamiliki wa shule kuchukua tahadhari na kuhakikisha wanafanya ukaguzi mara kwa mara kwa kuwatumia wataalamu wa masuala ya moto.

"Vyombo vya dola vinaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini kuweza kubaini vyanzo vya moto huo uliosababisha vifo, hofu kwa wafanyakazi, wanafunzi, wazazi pamoja kusababisha hasara kubwa,'' Amesema Msemaji huyo.

Aidha Jeshi la Polisi limeomba ushirikiano kutoka kwa wananchi ili kuendelea kuimarisha hali ya usalama na kuepusha majanga ya moto pamoja na vitendo vya uhalifu.
 

Zaidi tazama Video hapo chini