Thursday , 16th Oct , 2014

Zaidi ya asilimia 63 ya akina mama nchini Tanzania wamepatiwa dawa katika kampeni ya kutokomeza maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto nchini.

Mratibu wa mpango wa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto PMTCT, Dkt. Mikyomo Kajoka amesema leo jijini Dar es Salaam kuwa kampeni hiyo ina lengo la kupunguza maambukizi hadi kufikia asilimia 4.

Kwa mujibu wa Dkt. Kajoka idadi ya wanawake wenye virusi vya ukimwi imezidi kupungua ambapo takwimu zinaonesha kuwa asilimia 53 ya wanawake ndio wanaojifungua hospitalini,na kuwataka wanawake kuwa na tabia ya kujifungua hospitalini ili kuokoa maisha ya watoto.

Hata hivyo amewataka wanaume kuambatana na wake zao wakati wa mahudhurio ya kliniki wakati wa ujauzito ili kusaidia kumlinda mtoto asipatwe na maambukizi.

Wakati huo huo, serikali imetakiwa kutoa elimu ya mara kwa mara kwa vijana juu ya athari mbaya zinazoweza kujitokeza ikiwemo kupoteza maisha au kupata majeraha mabaya endapo atalisogelea lori la mafuta mara tu baada ya kupata ajali na kupinduka.

Ushauri huo umetolewa leo na wakazi wa jiji la Dar es salaam kufuatia kuwepo kwa matukio ya mara kwa mara ya wananchi kuwa na tabia ya kulifuata lori la mafuta mara baada ya kupata ajali kwa lengo la kuchukua mafuta.

Aidha wakazi hao wa jiji wamesema umasikini unaochangiwa na kipato duni miongoni mwa vijana wengi wa jijini Dar es salaam imekuwa ni chanzo kwa vijana hao kujiingiza katika majanga yasiyo ya lazima.