Friday , 17th Apr , 2020

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania bara (TPBL) imefafanua juu ya uwezekano wa kuongezwa kwa idadi ya wachezaji wanaofanyiwa mabadiliko pindi ligi hiyo itakaporejea.

Kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba

Ufafanuzi huo umekuja baada ya kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba kutoa pendekezo lake kwa Bodi ya Ligi kuruhusu kuongeza idadi ya wachezaji wanaofanyiwa mabadiliko kutoka wachezaji watatu hadi watano, endapo ligi itarejea mwezi ujao.

Cioaba ametoa ombi hilo kwa TFF, akiwa na malengo ya kuwasaidia wachezaji kujiepusha na majeraha, endapo Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) itarejea hivi karibuni.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo amefafanua kuhusu uwezekano wa suala hilo ambapo amesema kuwa ni changamoto kubwa kubadilisha kanuni kuelekea mwishoni mwa msimu huku akisisitiza ni vyema wazo hilo likajadiliwa wakati wa mabadiliko ya kanuni mwishoni mwa msimu.

"Mimi nafikiri tulichukue ili wakati wa uboreshaji wa kanuni zetu tuliwasilishe lakini sioni kama kuna hiyo nafasi katikati ya msimu. Kwahiyo tutakapotangaza maboresho ya kanuni ni vizuri tukalichukua hilo", amesema Kasongo.

Ligi Kuu ya Soka Tanzania bara VPL imesimamishwa tangu Machi 17 mwaka huu, kutokana na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) linaloendelea dunia nzima, na mpaka sasa haijajulikana kama itarejea baada ya muda huo wa mwezi mmoja ambao unaishia leo.