Monday , 9th Mar , 2020

Ikiwa imepita takribani miezi miwili tangu viongozi sita wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(DARUSO), kusimamishwa masomo yao tayari wamekwishapokea mashtaka yao na Machi 18 watakutana na kamati ya nidhamu ya chuo kwa ajili ya kusikilizwa.

Jengo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha biashara

Akizungumzo na EATV&EA Radio Digital, Rais wa Serikali ya wanafunzi Hamis Mussa, amesema kuwa japo tayari wamekwishapokea mashtaka yao, lakini bado hawana matumaini kama wataweza kuruhusiwa kuendelea na masomo.

"Tuko kwenye mchakato, tulipokea mashtaka kila mtu ya kwake na tuliyajaza kwa maandishi na tukayarudisha na Machi 18, 2020, tutaanza kusikilizwa na kamati ya nidhamu, tutakapoonana nao ndio tutajua kama tutaruhusiwa kuendelea, lakini kiukweli hadi sasa tupo njia panda" amesema Rais wa DARUSO.

Rais wa DARUSO pamoja na wenzake watano, walisimamishwa masomo yao Disemba 18, 2020, baada ya kutoa tamko la masaa 72 kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu wakishinikiza kulipwa mikopo yao.