
Matukio ya kimichezo yaliyotokea mwaka 2019
Katika tasnia ya michezo ni mengi yamefanyika ambayo kwa upande mmoja yameleta mafanikio katika tasnia ya michezo nchini na matukio mengine yameleta simanzi na masikitiko. Tunaanza kuyatazama matukio hayo kwa undani wake.
Uwekezaji Simba kuanza kufanya kazi: Ni muendelezo wa hatua ambayo ilianza tangu mwaka uliopita wa 2018 ambapo klabu ya Simba imeendeleza mchakato wa mabadiliko ya kimfumo.
Ikishuhudiwa kuajiriwa kwa CEO mpya kutoka Afrika Kusini, Senzo Mazingisa, ujenzi wa awamu ya kwanza ya uwanja wa mazoezi wa Bunju maarufu kama 'Simba Mo Arena' pamoja na uzinduzi wa kadi za kibenki za mashabiki wa klabu hiyo.
Hassan Mwakinyi kumchapa Mfilipino: Bondia anayekuja kwa kasi nchini kwa sasaa, Hassan Mwakinyo alimchapa Mfilipino, Arnel Tinampay kwa pointi, Novemba 30 katika pambano lililofanyika Jijini Dar es Salaam.
Pambano hilo liliweka rekodi ya kutazamwa na watu wengi zaidi nchini katika televisheni na mtandao, ambapo baada ya pambano kulizuka sintofahamu baina ya Mwakinyo na bondia mkongwe, Rashid Matumla kutokana na uchambuzi wake alioutoa kwenye mchezo huo.
Tanzania kufuzu AFCON baada ya miaka 39: Machi 23, 2019 timu ya taifa 'Taifa Stars' ilifanikiwa kufuzu michuano ya AFCON kwa mara ya kwanza tangu 1980 baada ya kuifunga Uganda mabao 3-0 Jijini Dar es Salaam.
Katika michuano yenyewe ya AFCON iliyofanyika nchini Misri, Taifa Stars iliondolewa hatua ya makundi ikiwa haijashinda mchezo wowote, ambapo ilipoteza mechi ya kwanza dhidi ya Senegal kwa kufungwa mabao 2-0 kabla ya kufungwa na Kenya mabao 3-2 na kisha kufungwa na Algeria mabao 3-0.
Itaendelea tena sehemu ya pili.