Friday , 20th Dec , 2019

Kufuatia taarifa zilizotolewa leo Disemba 20, 2019, na Mwanaharakati Bob Chacha Wangwe, zimeeleza kuwa Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti, amekamatwa kwa nguvu na watu watano ambao hawakuweza kutambulika mara moja maeneo ya Mwenge, jijini Dar es Salaam.

Mwanasheria kutoka LHRC, Tito Magoti

Akizungumza na EATV&EA Radio Digital, Bob Chacha Wangwe amesema kuwa yeye amepata taarifa za kutekwa kwa Tito Magoti, kutoka kwa ndugu wa karibu na kwamba hivi sasa wanafanya ufuatiliaji ili kujua undani wa tukio hilo.

"Mimi taarifa nimepata kwa mtu anayekaa naye, maana alipelekwa Mwenge na Dereva bodaboda, aliposhuka tu ikatokea gari aina ya Harrier wakatoka watu watano wakamkamata kwa nguvu na kumfunga pingu na kumuingiza kwenye gari na kuondoka naye, kwahiyo ikabidi yule bodaboda arudi nyumbani kutoa taarifa" amesema Bob Chacha Wangwe.

Kwa upande wake Afisa Habari wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Michael Valentine, amesema kuwa na wao bado wanafuatilia ili kujua ni kitu gani haswa kimempata maana hata simu yake ya mkononi haipatikani.

"Na sisi taarifa tumeziona na tunafuatilia kwa ukaribu tuweze kufahamu na tunaongea na ndugu zake, kwa upande wangu nimempigia simu na simu yake haipatikani, tunafuatilia tukijiridhisha tutatoa taarifa rasmi" amesema Michael.

Aidha EATV&EA Radio Digital, ilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni,Mussa Taibu ili kujua kama anazo taarifa hizi.

"Hapana mimi sina taarifa za Tito Magoti" amesema RPC Kinondoni.