Friday , 15th Nov , 2019

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), limesema kuwa moja ya sababu iliyopelekea kumfungia kufanya kazi za mziki, rapa Rosa Ree, ni pamoja na kitendo cha yeye kufanya kazi ya muziki nje ya Tanzania, bila kuwa na kibali cha Baraza hilo na kwamba anayo nafasi ya kukata rufaa ndani ya siku 30.

Msanii Rosa Ree

Akizungumza leo Novemba 15, 2019 na EATV & EA Radio Digital, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Onesmo Kayanda, amesema adhabu yake ipo katika maeneo mawili, ambayo ni ukosefu wa maadili na kitendo cha kutoka nje ya nchi kwenda kufanya kazi bila kupata kibali.

"Adhabu yake ipo katika maeneo mawili, moja ni maeneo ya maadili, mbili ni kitendo cha kutoka nje ya nchi kufanya kazi bila kibali cha Basata, ukishakuwa umesajiliwa mahali lazima ufuate sheria, kanuni, taratibu na miongozo, alivyokiuka maadili imempelekea kupata adhabu ya kulipa milioni 2 na kufungiwa kufanya kazi za sanaa kwa muda wa miezi 6" amesema Onesmo.

Aidha Kayanda ameongeza kuwa, "Lakini Basata inapofikia adhabu kama hiyo inakuwa imejaribu kumsikiliza mtu kwa muda mrefu na kuangalia yanayoendelea kufanyika katika sanaa yake, ila bado ana nafasi ya kukata rufaa ndani ya siku 30 kama ataona adhabu aliyotolewa ni kubwa au anaweza akamuomba Waziri anayejihusisha na sanaa aipitie au aifute endapo atajidhihirisha".