Thursday , 26th Sep , 2019

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amesema kuwa hana mahusiano mazuri na Mkuu wa mkoa huo, Ally Hapi kwasababu amekuwa akichukulia masuala ya Serikali kuwa ya kibinafsi na kutotambua nafasi yake katika mkoa huo.

Akizungumza leo Septemba 26, 2019 na EATV & EA Radio Digital, Msigwa amesema kuwa mara nyingi amekuwa akimzuia hata kuzungumza na wananchi wake, kitendo kinachoashiria yeye kutoheshimu maamuzi ya wananchi waliompa dhamana ya kuongoza jimbo hilo.

''Kimsingi mimi mahusiano yangu na RC Hapi hayako vizuri, kwanza amekuwa hataki kutambua kama mimi ni Mbunge wa hapo, hata shughuli za kiserikali zikifanyika jimboni kwangu yeye hataki niongee, kwahiyo mimi namuona kama mtoto hajui siasa ila atakua baadae atajifunza, kwasababu mwisho wa siku wananchi wanatufahamu ila haya yanapita na yana mwisho'', amesema Msigwa.

Akizungumzia kama kauli zinazotolewa na Mkuu huyo wa Mkoa dhidi yake zinamyumbisha kisiasa, Msigwa amesema yeye ataendelea kuyapuuza na hayawezi kumvunja nguvu na bado ataendelea kuongoza jimbo hilo.