Wednesday , 25th Sep , 2019

Mbunge wa Singida Mashariki kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Miraji Mtaturu, ameahidi kila mwaka atahakikisha anachangia sare za shule kwa wanafunzi 200 wa shule za msingi na sekondari pamoja na kulipia gharama mbalimbali za masomo kwa wanafunzi watakaofaulu kwenda

kidato cha tano kutoka shule za kata.

Mtaturu amesema kuwa licha ya serikali kuondoa gharama za ada mashuleni, lakini wapo wazazi wenye vipato vya chini, wanaoshindwa hata kumudu gharama za kuwanunulia watoto wao sare za shule.

''Nitakuwa nachangia sare za watoto 200, sekondari wanafunzi 100 na shule za msingi wanafunzi 100 kila mwaka nia na madhumuni yangu ni kuzisaidia familia ambazo zimekosa uwezo huo na mimi sasa niweze kuwasaidia watoto wao wapate haki ya msingi ya elimu'', amesema Mtaturu.

Mtaturu amewaagiza watendaji wa vijiji kuhakikisha wanazibaini familia zenye watoto waliofaulu kwenda kidato cha tano lakini wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na hali ya uchumi na kwamba wampelekee orodha ili kila mwaka ahakikishe anasaidia kulipa gharama kwa wanafunzi 10, wasichana wakiwa watano na wavulana watano.