Akitoa taarifa ya mwenendo wa soko leo Septemba 23, Meneja miradi wa soko hilo Emmanuel Nyalali amesema wakati thamani ya mauzo ikipanda, idadi ya mauzo ya hisa imeongezeka kutoka hisa Milioni 1.48 kwa juma lililotangulia na kufikia hisa milioni 590.93 juma lililoishia Septemba 20.
''Kwa ujumla ni kaunta moja ambayo ndiyo iliyoleta mauzo makubwa kiasi hicho, ni kaunta ya Vodacom iliyochangia asilimia 98.98 ya thamani ya mauzo ya hisa na asilimia 99.50 ya idadi ya hisa zote zilizouzwa sokoni'', amesema Nyalali.
Wawekezaji wa ndani walichangia asilimia 99 ya thamani ya mauzo yote ya hisa, huku wawekezaji wa nje wakichangia asilimia 99 ya manunuzi yote ya hisa.
Nyalali ameongeza kuwa thamani ya Soko la Hisa ilipanda hadi kufikia Shilingi Trilioni 19.03 ukilinganisha na thamani ya juma lililoishia Septemba 13 ambayo ilikuwa Trilioni 18.82, lakini pia thamani ya hatifungani imepanda na kufikia bilioni 45.24, ukilinganisha na mauzo ya bilioni 26.65 kwa juma lililoishia Septemba 13.

