Saturday , 21st Sep , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Dar ea salaam Mhe. Paul Makonda ameitisha kikao baina yake na watendaji wa Mkoa huo wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Mameya, Wakurugenzi wa Manispaa, Makatibu tawala na wakuu wa Idara ili wamueleze ni kitu gani kinachofanya miradi ya kimkakati ichelewe.

Paul Makonda

Hilo amelibainisha leo Septemba 21, 2019, wakati wa hafla ya kutoa zawadi kwa walimu, wanafunzi na shule zilizofanya vizuri katika taaluma na michezo, katika mkoa wa Dar es salaam.

Mkuu huyo wa mkoa amesema mkutano huo utafanyika Jumatano ya Septemba 25, 2019, katika ukumbi wa Karimjee, na mtendaji atakayebainika kusababisha uzembe huo atawajibishwa hapo hapo kwa mujibu wa sheria na wengine watazuiwa mishahara yao.

Ameitaja miradi hiyo ni kama Machinjio ya Vingunguti na Ufukwe wa Coco, ambayo imechelewa kutekelezwa licha ya Rais Dkt. John Magufuli kutoa fedha za miradi hiyo lakini fedha hizo zimeishia kukaa kwenye akaunti pasipo utekelezaji.

Aidha Makonda ametoa wito kwa Wizara ya Utumishi na TAMISEMI kutafuta njia bora ya kuwapata wakuu wa Idara wenye uwezo wa kuleta matokeo Chanya, tofauti na sasa ambapo wengi wao wamepanda na kuwa wakuu wa idara kwa kigezo cha kukaa kazini muda mrefu.

Hivi karibuni Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika machinjio ya Vingunguti na kukuta ujenzi ukisuasua licha ya serikali kutoa zaidi ya Bilioni 14 kwaajili ya ujenzi huo.

Katika ziara hiyo Rais aliwataka Mkuu wa mkoa, Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi wa Manispaa kuhakikisha wanamaliza ujenzi huo ndani ya miezi mitatu, huku akipiga marufuku kukusanya ushuru ambao kwa mwezi ulikuwa unafikia shilingili Milioni 100.