Saturday , 31st Aug , 2019

Moto mkubwa  ambao chanzo  chake hakijajulikana,  umezuka na  kuteketeza moja kati ya maghala matatu, ya kuhifadhia pamba katika kiwanda cha Sunflag kilichopo Mkoani Arusha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Jonathan Shanna

Akizungumza na EATV & EA Radio Digital, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Jonathan Shanna, amesema kuwa moto huo umeanza kuwaka kuanzia majira ya saa 7:00 mchana, ambapo hadi sasa Jeshi la  Zimamoto na Uokoaji,  linaendelea na juhudi za kuuzima moto huo.

''Taarifa za kuteketea kwa Ghala ni za kweli na hakuna madhara yoyote kwa binadamu,  lakini sasa hii Pamba inawaka kiaina, ukizima juu moto mwingine unaibuka chini, ukizima chini moto mwingine unaibuka juu, lakini Jeshi la Zimamoto liko hapa kwa pamoja tunajitahidi kuuzima, tunaomba Mungu moto huu usienee maeneo mengine ukaleta athari zaidi'', amesema RPC Shanna.

Kamanda Shanna ameongeza kuwa, changamoto nyingine inayowakabili ni kutokuwepo kwa vyanzo vya maji vilivyokaribu na eneo hilo ili kuweza kurahisisha zoezi la uzimaji na kwamba zoezi litakapokamilika watatoa tathimini ya hasara iliyopatikana.