
Mwenyekiti wa bodi ya Parole nchini na Mwenyekiti wa Chama Cha Tanzania Labour Party (TLP), Agustino Mrema, na Mbunge wa Vunjo James Mbatia.
Mbunge wa sasa Jimbo la Vunjo ni James Mbatia ambaye alishika nafasi hiyo baada ya kuungana na vyama vingine vya upinzani ikiwemo CUF, Chama Cha Demiokrasia na Maendeleo CHADEMA, pamoja na NLD.
Mrema amedai James Mbatia alihamia Vunjo kwenye ngome ya upinzani, kwa lengo la kumuondoa yeye, lakini si kupambana kwenye majimbo ambayo CCM inaongoza.
"Vyama hivi vya UKAWA ndiyo niliviona Vunjo mimi nikiwa mpinzani wakanikataa na wakanichangia kama mpira wa kona, badala ya kupambana na CCM wakapambana na mimi, na walimleta Mbatia agombee Vunjo ili kuning'oa na kunimaliza kisiasa na wamefanikiwa" - Mrema.
"Huwezi kuhamia Vunjo kwa lengo la kunitoa mimi ambaye ni mpinzani mwenzako halafu ukiangalia historia yangu ni kubwa sana kwenye nchi hii, badala ya kuona ni namna gani ya kushirikiana na mimi lakini walining'oa" amesema Mrema.
Agustino Mrema alishawahi kuwa Waziri wa mambo ya ndani ya nchi ambaye alikuwa maarufu kwa namna ya utendaji kazi wake na kumfanya kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 kuwa Mgombea Urais wa chama cha upinzani nchini ambaye alipata kura zaidi ya milioni 1.