Friday , 14th Dec , 2018

Kumekuwa na tetesi za muda mrefu juu ya usajili wa mlinzi wa kati kisiki kutoka klabu ya Napoli, Kalidou Koulibaly ambaye amekuwa kwenye rada za Manchester United.

Kalidou Koulibaly

Vyanzo viwili tofauti vinasema kwa upande mmoja kwamba klabu hiyo iko tayari kutumia £ 100m kwa miamba hiyo kwaajili ya kumnasa Koulibaly, na  kwamba Jose Mourinho hafurahishwi na namna mchakato wa uhamisho huo unavyokwenda taratibu, kwani anataka dili hilo likamilike mapema mwezi Januari.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo nchini Uingereza, Man United inapanga kumfanya nyota huyo wa timu ya taifa ya Senegal Senegal,  kuwa ndiye mlinzi wa gharama kubwa zaidi katika historia ya soka kwa ambayo itavunja rekodi  ya sasa ya £ 75m iliyowekwa na Liverpool wakati ilipomsajili Virgil van Dijk takribani mwaka mmoja uliopita.

Tetesi zimekwenda mbali zaidi ambapo inasemekana kuwa tayari ofa mbili za Man United kwa mchezaji huyo zimekataliwa na Napoli, ambapo sasa Jose Mourinho anajipanga kupeleka ofa ya tatu. 

Mourinho ana shinikizo la kutofanya usajili mzuri wa majira ya joto msimu huu, ambapo alifanikiwa kusajili wachezaji watatu pekee, Diogo Dalot, Fred na mlinda mlango Lee Grant huku mwenyewe akikiri kuwa hakuridhishwa na usajili huo kwani alihitaji wachezaji wengine muhimu lakini hakutimiziwa na bodi ya wakurugenzi chini ya Mtendaji Mkuu, Ed Woodward.

Man United itashuka dimbani Jumapili dhidi ya wenyeji Liverpool katika mchezo wa EPL. Man United inakamata nafasi ya sita ya msimamo wa EPL kwa alama 26 huku Liverpool ikiwa kileleni kwa alama zake 42.