Wednesday , 30th Jul , 2014

Makamu wa Rais Dkt. Mohamed Gharib Bilal, amewataka waislam nchini kusherehekea Sikukuu ya Eid El Fitri kwa amani na utulivu na kutofanya matendo maovu yasiyompendeza Mwenyezi Mungu kwa lengo la kudumisha amani.

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt Mohammed Gharib Bilal.

Dkt. Bilal amesema hayo leo Jijini Dar es Salaam mara baada ya kushiriki katika swala ya Eid El Fitri iliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais amesema kuna nchi ambazo zimeshindwa kusheherekea Sikukuu ya Eid El Fitri kutokana na kutokuwa na amani katika nchi zao hivyo ni vema amani iliyopo hapa nchini ikaendelea kudumishwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Wakati huo huo, taasisi ya Kimataifa inayojishulisha na kuwabadilisha vijana kifikra na kuwa na mtazamo wa kimaendeleo zaidi (IYF) imewahakikishia vijana wa Tanzania kuwapa elimu itakayowasaidia kubadili fikra zao na kujiajiri wao binafsi badala ya kuendelea kuwa tegemezi.

Mkurugenzi Mkazi wa IYF nchini Tanzania Jeon Hee Yong amesema taasisi hiyo kwa sasa imeweza kuwafikia zaidi ya vijana elfu 3 ambao kupitia kambi maalum za vijana wameweza kubadilisha fikra zao na kuwa na mawazo ya kujiendeleza.

Kwa upande wao baadhi ya vijana wanaoshiriki kambi mbalimbali za IYF wamesema wameweza kupata elimu ambayo kwa sasa nao wanaitumia kuwaelimisha wenzao kwa lengo la kuwabadilisha kifikra ili hapo baadaye wawe vijana wenye kujitambua katika ulimwengu wa sasa.