Kushoto ni mchezaji Fatuma Issa akiwa na Rais wa TFF Wallace Karia.
Akiongea na www.eatv.tv Fatuma maarufu kama Fetty Densa, amesema mipango yote inaenda sawa na akirejea tu jijini Dar es salaam kutoka Kigali Rwanda ambako yupo na timu ya taifa ya wanawake, atakaa kidogo nchini kisha ataelekea Sweden tayari kwa kuanza maisha mapya ya soka la kulipwa.
''Nimefurahi kuwa mchezaji bora kwenye michuano hii sina hata cha kusema ila imeniongezea kitu hata mipango yangu ya kwenda kucheza soka Sweden wiki chache zijazo itatimia kirahisi maana tayari uwezo wangu unatambulika'', - amesema.
Mchezaji Fatma Issa.
Hata hivyo Fatuma amegoma kuweka wazi ni timu gani anakwenda kuchezea kwa kile alichoeleza kuwa kuna vitu vinakamilika na ataweka wazi kwa Watanzania kabla ya kuondoka ili wamuombee akafanye vizuri na kuiwakilisha vizuri Tanzania.
Jana jioni Julai 27, 2018 Fatma alitangazwa kuwa mchezaji bora wa michuano ya soka kwa wanawake kwenye ukanda wa Africa Mashariki na Kati 'CECAFA Women Challenge' huku Kilimanjaro Queens ikiibuka mabingwa kwa kuwa na pointi 7 ambazo hazikufikiwa na timu nyingine.