Msemaji wa mamlaka ya usimamizi wa huduma za hifadhi ya jamii nchini Tanzania (SSRA) Bi. Sarah Kibonde Msika.
Msemaji wa SSRA Bi. Sarah Kibonde Msika, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam na kufafanua kuwa sheria iliyopo haitoi fursa ya kuwepo fao la kukosa ajira ambalo alisema hata hivyo ni muhimu kwani linaendana na maazimio ya shirika la kazi ulimwenguni - ILO.
Kwa mujibu wa Bi. Kibonde, idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za hifadhi ya jamii hivi sasa ni ndogo kwani kati ya watu milioni 22 ambayo ndio nguvu kazi halisi ya taifa, ni chini ya watu milioni mbili tu ndio wanatumia huduma za hifadhi ya jamii na kwamba kuna haja ya idadi hiyo kuongezeka.
Bi. Kibode Kibonde amefafanua kuwa katika kuhakikisha idadi hiyo inaongezeka, SSRA imekuwa ikiendesha zoezi la elimu kwa umma ambapo mpaka sasa watu zaidi ya elfu kumi wamepata elimu juu ya umuhimu wa kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii, kutoka mikoa zaidi ya kumi nchini.
Aidha, msemaji huyo wa SSRA amewataka waajiri kutoa fursa kwa wafanyakazi wao kujiunga na mfuko wowote wa hifadhi ya jamii wanaotaka, huku akiitaka mifuko ya hifadhi ya jamii kuacha kutumia mbinu chafu katika kusajili wanachama, ikiwa ni pamoja na mifuko hiyo kuchafuana yenyewe kwa yenyewe.