Friday , 26th May , 2017

Klabu ya Yanga imepigwa faini ya jumla ya shilingi milioni 5 kwa makosa mbalimbali iliyobainika kuyafanya kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa ligi kuu Tanzania Bara msimu uliomalizika wa 2016/17 huku wachezaji wake watatu wakisimamishwa

Adhabu hiyo ni sehemu ya uamuzi wa adhabu mbalimbali kutoka Kamati y Saa 72 uliotangazwa leo baada ya kupitia michezo mbalimbali za ligi hiyo ambapo kwa upande wa Yanga umezingatia kuwa klabu hiyo imekuwa ikirudia rudia baadhi ya makosa hasa kosa la kutoingia katika vyumba vya kubadilishia nguo. Adhabu hizo ziko kama ifuatavyo.......

Mechi namba 236 (Mbao FC 1 Vs Yanga 0).

Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kupita mlango usio rasmi katika mechi hiyo iliyofanyika Mei 20, 2017 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Pia Yanga imepigwa faini ya sh. 1,500,000 (milioni moja na laki tano) kwa kutoingia vyumbani na faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kuonyesha vitendo vinavyoashiria ushirikiana.

Katika mchezo huo pia mashabiki wa Yanga walivunja uzio wa ndani (fence) wa upande wa Magharibi wakati wakiingia uwanjani kusherehekea ubingwa wa timu hiyo. Hivyo, klabu ya Yanga imeagizwa kulipa gharama za uharibifu huo uliofanywa na mashabiki wake.

Nayo klabu ya Mbao FC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na mashabiki wake kuingia uwanjani kushangilia baada ya timu yao kupata ushindi.

Pia wachezaji Deus Kaseke, Simon Msuva na Obrey Chirwa wa Yanga wamesimamishwa kucheza mechi za Ligi Kuu wakati wakisubiri suala lao la kumsukuma na kumwangusha Mwamuzi Ludovic Charles katika mchezo huo dhidi ya Mbao FC, kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Naye Mwamuzi Ludovic Charles amepewa onyo kali kwa kutodhibiti vizuri mchezo huo.

Vitendo vilivyoashiria ushirikina katika mchezo wa Yanga na Mbao FC, Kirumba Mwanza

Yanga pia imejikuta ikipigwa faini nyingine kama ifuatavyo.

Mechi namba 206 (Yanga 1 Vs Toto Africans 0).

Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na timu yake kutoingia vyumbani wakati wa mechi yake dhidi ya Toto Africans iliyochezwa Mei 9, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi namba 231 (Yanga 2 Vs Mbeya City 1).

Timu zote mbili hazikupita kwenye mlango rasmi wakati wa kuingia uwanjani katika mechi hiyo iliyochezwa Mei 13, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Hivyo, kila klabu imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kitendo hicho.

Pia klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kutoingia vyumbani kwenye mechi hiyo.

Mbali na adhabu hiyo, kamati hiyo imetangaza adhabu nyingine kama ifuatavyo

Mechi namba 225 (JKT Ruvu 0 Vs Majimaji 1).

Timu ya Majimaji haikuingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi hiyo iliyofanyika Mei 13, 2017 katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na hivyo klabu hiyo imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja).

Mechi namba 230 (Kagera Sugar 2 Vs Mbao FC 0).

Klabu ya Mbao imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na timu yake kutoingia vyumbani wakati wa mechi hiyo iliyochezwa Mei 13, 2017 katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.