Kocha wa Ruvu Shooting, Malale Hamsini
Afisa habari wa Ruvu Shooting Masau Bwire amesema, Kocha Malale tayari ameshawasili kambini Mabatini Mkoani Pwani ambapo Desemba 05 ataanza rasmi majukumu aliyokabidhiwa ya kukinoa kikosi hicho kama kocha Mkuu.
Masau amesema, uongozi umefikia uamuzi huo wa kumchukua Kocha Malale kutokana na uwezo wake mzuri wa kufundisha mpira kama unavyopambanuliwa na mafanikio makubwa katika timu alizowahi kuzifundisha.
"Malale ni kocha mzuri, ameifundisha timu ya JKU kwa mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuipandisha hadi ligi kuu ya Zanzibar mwaka 2013, msimu wa 2014 ikiwa mikononi mwake ilishika nafasi ya pili katika Ligi hiyo ya Zanzibar, aliifikisha timu hiyo nusu fainali ya mashindano ya kombe la mapinduzi, pia aliiwezesha kutwaa ubigwa wa mashindano ya majeshi mwaka 2013 jijini Dar es salaam,"amesema, Masau.
Malale ambaye pia ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes alianza rasmi kazi ya ukocha mwaka 2004 akiifundisha kwa mafanikio makubwa timu ya Ngome na baadaye timu ya Faru Jumbi.