Sunday , 27th Nov , 2016

Chama cha Wananchi CUF chini ya uongozi wa Prof Lipumba, kimefanikiwa kuyakamata magari sita kati ya saba iliyokuwa inayatafuta ambayo wamiliki wake walikaidi agizo la Mwenyekiti wa chama hicho la kurejeshwa kwa mali zote zilizo nje ya ofisi.

Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF Taifa, Abdul Kambaya

Akizungumza na wanahabari katika makao makuu ya ofisi hizo Buguruni jijini Dar es Salaam, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF taifa Bw. Abdul Kambaya amesema magari hayo yamekutwa yamefichwa nyumbani kwa kada mmoja wa Chama kimoja maarufu nchini pasipo sababu zinazoeleweka.

Kukamatwa kwa magari kunafuatia mpasuko unaotokana na tofauti ya kiuongozi ndani ya chama hicho ambapo upande mmoja unamtii Katibu Mkuu wake Maalim Seif Sharif Hamad huku upande mwingine ukimtii Mwenyekiti wake Profesa Ibrahim Lipumba.

Tofauti hiyo ndiyo iliyozaa wazo la kurejeshwa kwa mali zote za chama hasa baaada ya kubainika kuwa sehemu kubwa ya mali hizo ipo mikononi mwa viongozi waandamizi.

Mapema mchana leo, Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad amewaambia wanahabari kuwa chama hicho kinapitia msukosuko mkubwa wa kiuongozi na kuwataka wanachama wake waimarishe umoja kwani mwisho wa yote chama hicho kitaendelea kuwa imara kama ilivyokuwa miaka iliyopita.

________________
Kumpigia KURA msanii unayempenda kwenye #EATVAwards Bofya hapa https://www.eatv.tv/awards