Friday , 9th May , 2014

Waziri wa Mali asili na Utalii nchini Tanzania Lazaro Nyalandu amesema hadi kufikia mwisho wa mwezi ujao serikali itakuwa imeajiri jumla ya askari wa wanyamapori 430 kwa lengo la kukabiliana na ujangili.

Waziri wa maliasili na utalii nchini Tanzania, Lazaro Nyalandu.

Aidha, waziri Nyalandu amesema ajira hizo mpya za askari wa wanyamapori zitaenda sambamba na ununuzi wa helikopta tatu zitakazotumika kufanya doria za mara kwa mara katika hifadhi za taifa za wanyamapori nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mh. Nyalandu pia ametangaza kuanzisha mamlaka mpya ambayo itajulikana kama mamlaka ya wanyamapori Tanzania ambayo makao makuu yake yatakuwa mkoani Morogoro na katika kufanikisha hilo amewataka wahifadhi wote kujiandaa kwa kwenda kufanya kazi mkoani humo.

Amesema ajira za askari wa wanyama pori zitaongezeka hadi kufikia mwezi wa saba na kufikia askari 930 lengo likiwa ni kuhakikisha vita dhidi ya ujangili inadhibitiwa katika hifadhi za wanyamapori zote za hapa nchini.