Tuesday , 27th Sep , 2016

Ndege mpya ya PILI iliyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kutumiwa na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) imetua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam ikitokea nchini Canada ilikotengenezwa.

Ndege ya pili ya Bombadier Q400 iliyonunuliwa na serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) ikipata Saluti ya maji (Water Canon Salutation) mara tu baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Septemba 27, 2017 ikitokea Canada ilikotengenezwa.

Ndege hiyo aina ya Bombadier Dash - 8 Q400 NextGen imetua majira ya saa 6:50 Mchana na kisha kupatiwa heshima maalum kwa kumwagiwa maji na magari ya zimamoto (Water Salute).

Akizungumza baada ya kuwasili kwa ndege hiyo Katibu Mkuu Uchukuzi Dkt. Leonard Chamriho amesema baada ya kuwasili kwa ndege zote mbili uzinduzi rasmi utafanyika kesho Jumatano kuanzia saa 3.00 asubuhi ambapo mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Dkt. Chamriho amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi wa ndege hizo.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) Mhandisi Ladislaus Matindi amesema ATCL imejipanga kuingia katika soko la ushindani na kuwaahidi watanzania huduma nzuri na bora katika kuhakikisha wanasafiri kupitia sekta hiyo ya anga,kwa usalama na bei nafuu.

Ndege hii ya pili imewasili ikiwa ni wiki moja baada ya ndege ya kwanza iliyowasili tarehe 20 Sept 2016.

Katibu Mkuu Uchukuzi Dkt Leonard Chamriho na viongozi wengine wakielekea kwenye Ndege ya pili ya Bombadier Q400 iliyonunuliwa na serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege la Taifa (ATCL)