Sky Walker
Akizungumza na EATV, Sky Walker amesema amepata faraja kubwa baada ya kuanzishwa kwa EATV AWARDS, baada ya kukaa kwa muda mrefu na tuzo moja.
"Nimepata faraja sana mwaka huu tumepata tuzo kubwa zaidi, unajua historia ya EATV imekuwa na mchango mkubwa kwenye tasnia ya muziki, kwa wao kuanzisha tuzo ni jambo kubwa na zimekuja wakati mzuri, kwani kwa muda mwingi tulikuwa na tuzo moja na ambayo hata hatujui kama mwaka huu itakuwepo, kama zisingekuja mwaka huu ungepita kapa", alisema Sky Walker.
Sky Walker ambaye pia ni mtu anayejihusisha na masuala ya media, amesema tuzo hizo zitaleta changamoto kwenye muziki wa Tanzania na kuleta hamasa kubwa kwa wasanii kufanya kazi zenye ubora.
"Siku zote tuzo zina kazi ya kuleta motisha, naamini zitaleta changamoto, na kwa jinsi mchakato ulivyo wa msanii kujisajili mwenyewe moja kwa moja, na team ya academy kukaa kuchagua kazi bora, na kisha kurudishwa kwa wananchi kupigiwa kura, ina urasmi zaidi, lakini pia namna ya kupata mshindi, mshindi akipatikana atajua nimepata hii tuzo kwa kuihangaikia", alisema Sky Walker.
EATV AWARDS ni tuzo kubwa za kwanza kuanzishwa kwenye tasnia ya sanaa, ambazo zinahusisha moja kwa moja wasanii wa nchi za Afrika Mashariki, zikihusisha wasanii wa filamu na muziki.