Halima Mdee
Mheshimiwa Mdee ameyasema hayo wakati akizungumza na East Africa Radio na kuongeza kuwa katika kupambana na hali hiyo tayari wameanza kufanya jitihada za makusudi za kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwa gharama nafuu.
Amesema katika kuhakikisha wanapunguza kero hiyo ya kukosekana kwa maji safi na salama wameanza utaratibu wa kutafuta maeneo yakujenga vibanda vya kuuzia maji kwa bei nafuu na gharama ambazo mtanzania wa kawaida anaweza kuzimudu kulingana na uwezo wake, hivyo ameiomba DAWASCO kutoa ushirikiano kwa viongozi hao ili kuweza kufanikisha zoezi hilo kwa wananchi.
Kwa upande wa swala la afya Mdee amesema kina mama wengi wamekuwa na jukumu la kuwahudumia wagonjwa, hivyo wameanzisha mpango maalum wa kuwapatia bima maalumu ya afya ambayo inachangiwa nusu kwa nusu baina ya serikali na wananchi wenyewe, sambamba na maboresho ya huduma nyingine za afya hasa ya mama na mtoto.
Wakati huohuo Mheshimiwa Mdee amesema kuhusu mikopo ya kinamama na vijana ambayo kila halmashauri inatakiwa itenge 10% ya mapato yake kwaajili ya makundi hayo, kwa halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa mwaka wa fedha 2016/2017 wametenga bilioni 3 kwa madhumuni ya kuzipeleka kwa vijana nusu na kina mama nusu, lengo likiwa ni kila kata iweze kupata shilingi milioni 200 ya kukopesha watu wake kwa njia ya mfumo wa kibenki.
Kwa upande wa vijana amewataka wachangamkie fursa mbalimbali za ajira zinazotolewa na serikali kwajili ya kujiingizia vipato vyao wenyewe na familia zao.
Kuhusu jina lake kutumika katika kutapeli watu kwa njia ya mtandao, Mdee amevitaka vyombo vya Dola vyenye dhamana ya kusimamia mitandao nchini visimamie haki na sheria ya mitandao kama inavyoelekeza kwani bado anakutana na changamoto mbalimbali kutoka kwa watu waliotapeliwa kupitia jina lake wakimtuhumu kuwatapeli.