Friday , 19th Aug , 2016

Kundi lililofuzu usaili wa kwanza kabisa wa Dance 100% mwaka 2016 uliofanyika katika viwanja vya Leaders Club Jijini DSM na kuishia hatua ya robo fainali limesema bado halijakata tamaa na kwamba linakwenda kujipanga kwa ajili ya mashindano yajayo.

Kundi la Mafia Crew.

Akizungumza na EATV Mwenyekiti wa kundi hilo Mauzu Issa amesema walijipanga kwa kadri ya uwezo wao lakini bahati haikuwa yao mwaka huu ila wataendelea kujiimarisha ili mwakani waweze kuchukua ushindi wa shindano hilo.

“Sisi tumeshiriki kwa mara ya kwanza na kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali japo kuna makundi yalifika hadi nusu finali mwaka jana na mwaka huu hawakuweza kufua dafu hiyo inaonesha sisi tupo makini na tukikaza hakika mwaka ujao tunaondoka na ushindi” Amesema Mauzu.

Mauzu ameongeza kuwa jambo ambalo limewafelisha kutinga hatua ya nusu fainali ni ubunifu waliojipanga wao wakadhani kwamba wapo juu kumbe kuna makundi mengine wamejipanga zaidi na kwa kutizama EATV wataweza kufahamu hadi mwisho ni mambo gani wanayakosa ili waweze kuongeza juhudi.

Kwa upande wake mmoja wa majaji wa shindano hilo Jaji Khalila amewataka washiriki ambao watashindwa kwa kutofikia vigezo wasikate tamaa bali waendelee kufanya sanaa katika maeneo yao na kushiriki shughuli za kijamii jambo ambalo litawafanya waimarike zaidi.

Shindano la Dance100% linasubiri hatua ya nusu fainali ambapo hatua ambazo zimepita zinaoneshwa kupitia EATV pekee Jumapili kwa udhamini maridhawa wa VODACOM na COCA-COLA

Tags: