Wednesday , 13th Jul , 2016

Wakazi wa kijiji cha Mindola, kata ya Ilindi wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma, wamewatimua wenyeviti wa vitongoji vitatu kijijini hapo kwa tuhuma za wizi wa mbao 108 mali ya kijiji.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana (aliyevaa sweta) akikagua maendeleo ya utengenezaji madawati kwenye karakana zinazotengeneza madawati

Wakazi hao wamefanya maamuzi katika mkutano mkubwa wa hadhara ambako walidai viongozi hao waliiba mbao hizo zilizolenga kutengeneza madawati ya shule.

Katika mkutano huo uliokuwa chini ya mwenyekiti wa kijiji Denisi Ndolosi, wananchi walikataa kutoa msamaha kwa viongozi hao baada ya serikali ya kijiji kutaka wasamehewe na wasitajwe jambo lililopelekea kuanza kwa vurugu wakitaka serikali yote ijihuzuru.

Awali ofisa mtendaji wa kijiji hicho Talita Njamasi, alitoa taarifa kuwa viongozi hao walikiri kosa lao na hadi juzi walikwisharejesha mbao 105 ambazo zilikuwa kwa fundi kwa ajili ya kutengeneza madawati.

Njamasi amesema uamuzi wa kupelekea mbao hizo kwa fundi hata kabla ya kuitisha mkutano, ulitokana na msukumo aliokuwa akipewa kutoka halmashauri kuhusu utengenezwaji madawati ambayo shule yao inadaiwa jumla ya madawati 67.

Kauli hiyo ilionekana kupingwa na wajumbe na hasa kitendo cha kiongozi wa sungusungu Joel Mbona alipokuwa akiwatetea waharifu na kukataa kuwataja kwa majina huku akiwatishia wanaohoji kwamba angewaweka ndani.

Mmoja wa wakazi hao Magreth Madelemu, alitaka wezi wa mbao hizo watajwe kwa majina hadharani na wasimame kutubu kabla ya uamuzi wa wanakijiji jambo ambalo lililoungwa mkono na mkutano.

Baada ya kibano hicho, mwenyekiti wa kijiji aliwataja wenyeviti wa vitongozi walioiba mbao kuwa ni William Mguji wa Kitongoji cha Kawawa, Jackson Mazoya wa kitongoji cha Azimio na Hamisi Nhembo wa kitongoji cha Miganga’a na mjumbe mmoja wa serikali na mwananchi wa kawaida ambao majina yao hayakupatikana.

Imeelezwa katika mkutano huo kuwa, watuhumiwa walichukua mbao hizo na kugawana wenyewe badala ya kuelekeza katika mpango uliokuwa umelengwa wa madawati.