Wednesday , 6th Jul , 2016

Kutokana na kukithiri kwa vitendo vya kihalifu katika maeneo ya Kata ya Kawe wananchi wa maeneo hayo wameiomba serikali kuwajengea Hospitali maalum kwa ajili ya kuwatibu na kuwahifadhi waathirika wa madawa ya kulevya wanaoishi katika kata hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi Diwani wa Kata ya Kawe Jijini Dar es salaam Muta Rwakatare amewaambia waandishi wa habari kutokana na kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wakazi wa maeneo hayo, yakuwepo kwa vitendo vya kihalifu katika kata hiyo amesema uchunguzi uliofanyika unaonyesha wengi wanaofanya vitendo hivyo vya kihalifu ni wale ambao wanatumia madawa ya kulevya.

Diwani Rwakatare amesema huduma zinazotolewa kwa sasa katika Hospitali ya Kawe kwa ajili ya watumiaji wa madawa ya kulevya hazikidhi mahitaji kutokana na vitendo hivyo kuendelea kushamiri katika kata hiyo na baadhi ya wananchi wanawasaidia waalifu hao kwa kuwaficha.

Ameiomba jamii ya watanzania kuhakikisha wanawafichua waalifu wa vitendo hivyo ili kunusuru maisha ya watu wengi hasa vijana, pia serikali kwa kushirikiana na jamii iwawezeshe kimitaji na elimu vijana ili kujikimu kimaisha tofauti na kutegemea biashara hiyo haramu ya madawa ya kulevya ambayo kama haitadhibitiwa taifa litapoteza nguvu kazi kubwa ya baadaye.