Saturday , 4th Jun , 2016

Kwenye mpira lolote linaweza kutokea! Huo ni usemi ambao Taifa Stars inaingia nao Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikipiga hesabu kali za kuikabili Misri kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2017 zitakazofanyika nchini Gabon.

Kikosi cha timu ya soka ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars kinashuka dimbani jioni ya hii leo Juni 04 mwaka huu katika uwanja wa taifa kuvaana na wageni Mafarao wa Misri kuwania tiketi ya kufuzu kwa michuano ya mataifa ya Afrika AFCON 2017 fainali zake zikipigwa nchini Gabon.

Ni ushindi pekee na mahesabu kwa Stars ndiyo kitu kitakachowasaidia kufufua mbio za kuelekea nchini Gabon na si matokeo mengine yoyote kati ya matatu ya mchezo wa soka.

Japo kuna msemo katika soka kuwa lolote linaweza kutokea na mpira ni dakika 90 na mwingine ule wa mgeni njoo mwenyeji apone hilo linaweza kuwa jambo ambalo si rahisi kutokana na aina ya timu na hali ilivyo katika msimamo wa kundi G ambalo Stars ipo ikiwa nafasi ya tatu kwa alama moja, huku Misri wao wakiongoza wakiwa na alama 7 wakifuatiwa na Nigetia ambao wanaalama mbili.

Stars inakabiliwa na mtihani mgumu na mrefu mbele ya Mafarao hao wa Misri huku ikihitaji si kingine ni ushindi tena mnono wa si chini ya mabao 3-0 ama zaidi ili kufufua mbio hizo za kuelekea Gabon mwakani.

Endapo Stars ambayo inanolewa na makocha wazawa Boniface Mkwasa na Hemed Morocco wakishauriwa na mkuu wa ufundi Abdalah Kibaden wataibuka na ushindi basi watakuwa wamefufua matumaini ya Watanzania kuiona fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza ikiwa imepita taklibani miaka 36 tangu timu hiyo ilipofanya hivyo mnamo mwaka 1979 na kucheza fainali zake mwaka 1980 zilizofanyika Lagos Nigeria.

Benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo wameapa kufia uwanjani na kuhakikisha ushindi wa aina yoyote unapatikana kabla ya timu hiyo kwenda kumaliza kazi ugenini dhidi ya Super Eagles ya Nigeria Septemba 3 mwaka huu.

Mungu Ibariki Taifa Stars ,Mungu ibariki Tanzania.