
Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, wakiwa ndani ya basi la UDART katika Kituo cha Magomeni
Mapema asubuhi katika vituo vya kupandia usafiri huo kumekuwa na misururu mirefu ya wasafiri wakikata tiketi ili kuwahi katika shughuli zao za kila siku, huku wengi wao wakisema hali hiyo imechangiwa na mashine kukwama mara kwa mara na kufanya zoezi hilo kwenda taratibu.
Usafiri huo unaoanzia Kimara mwisho na kupitia Ubungo kuelekea Kariakoo pamoja na Kivukoni, Mabasi yenye uwezo wa kubeba abiria 150 kwa mabasi makubwa na 90 kwa mabasi ya uwezo wa kati hii leo yameonekana kuwa mengi huku yakiwa na idadi ndogo ya abiria ukilinganisha na juma lililopita wakati wa yakifanya majaribio.
Mwandishi wetu akizungumza na baadhi ya abiria akiwemo Seleman Mkumbo pamoja na Donald Urio wamemwambia kuwa wamelazimika kutembea kutoka kituo kimoja kwenda kingine ili kukata tiketi kutokana na mashine kuharibika huku wakisema mfumo wa malipo kwa njia ya kadi uharakishwe ili kuepuka usumbufu uliojitokeza hii leo.
Akizungumzia kasoro hizo Msimamizi wa Kituo cha katikati ya Jiji Joshua Mushi anasema wanaendelea kushughulikia dosari zilizojitokeza katika mashine za kukatia tiketi ili siku zijazo usafiri huo uwe na ufanisi zaidi.