Monday , 16th May , 2016

Shirikisho la Soka nchini TFF limewataka wasimamizi wa michezo ya mwisho hususani kwa timu zinazowania nafasi mbalimbali katika ligi kuwa makini kuepusha upangaji wa matokeo.

Afisa habari wa TFF Alfredy Lucas amesema, katika michezo hiyo ambayo Yanga tayari ni Mabingwa lakini kwa upande wa nafasi ya Pili ushindani upo kwa upande wa Azam FC ambayo ilikata rufaa mbayo bado haijajulukana mpaka sasa lakini inapointi 63 huku Simba ikiwa na pointi 62.

Lucas amesema, katika zawadi za Ligi Kuu mdhamini hutoa hadi atakayekuwa katika nafasi ya nne ambayo inawaniwa na Tanzania Prisons yenye pointi 48 huku mtibwa Sugar ikiwa na Pointi 47 hivyo anaamini ushindani utakuwa wa hali ya juu katika kufunga pazia la Ligi huku kila timu ikihitaji kujiweka katika nafasi nzuri.

Kwa upande wa timu tano zilizo katika hatari ya kushuka daraja huku Coastal Union ikiwa tayari imeshashuka daraja, Lucas amesema bado timu mbili zinatarajiwa kuungana na Coastal Union kushuka daraja huku timu zote tano zikiwa zimepishana pointi moja moja.

Lucas amezitaja timu hizo kuwa ni African Sports, Mgambo, Kagera Sugar, JKT Ruvu na Toto African ambapo zote zitaamuliwa katika mchezo wa mwisho.

Katika michezo ya mwisho timu zote zitashuka kupambana kwa siku moja ambapo vita zaidi itakuwa kwa timu zinazowania nafasi ya pili mpaka ya nne huku zilizo katika hatari ya kushuka daraja nazo zikipambana kujinasua na hatari hiyo.

Katika michezo hiyo Mgambo ambayo ipo katika hatari ya kushuka daraja itakuwa ugenini Uwanja wa Chamazi kupambana na Azam FC ambayo inawania nafasi ya pili katika Ligi Kuu huku JKT Ruvu ambayo pia ipo katika hatari ya kushuka ikiwa ugenini Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ikicheza dhidi ya Simba SC ambayo nayo pia ipo katika vita ya kupambana kuwania nafasi ya pili.

Kwa upande wa African Sports ambayo pia inahitaji kujinasua ili kubaki katika Ligi Kuu itakuwa ugenini Uwanja wa Manungu Turiani pia kujaribu bahati yao dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo nayo pia inapambana kuhitaji nafasi ya nne katika msimamo huku Tanzania Prisons ambayo pia inawania nafasi ya nne ikiwa ugenini Uwanja wa Mkwakwani Mkoani Tanga kupambana na Coastal Union ambayo imeshashuka daraja.