Thursday , 5th May , 2016

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia Frowin Peter Mbwale, Mkazi wa Kawe jijini Dar es Salaam, kwa tuhuma za mauaji ya mke wake pamoja na mtoto wao ambao walikutwa wamuawa kwa kuchinjwa shingoni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Boniveture Mushongi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Boniveture Mushongi, amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa na mwenzake jana usiku maeneo ya Zinga wakati akijaribu kutoroka kufuatia taarifa zilizotolewa na wananchi wa eneo hilo.

Taarifa ya Polisi imeeleza kuwa Jana majira ya saa kumi na nusu jioni kwenye vichaka vya Kaole, Kanda ya Dunda wilayani Bagamoyo, Mtuhumiwa huyo akiwa na mwenzake Rajabu Juma Mkazi wa Makongo waliwaua Oliver Erasto na Emannuel Frowin kwa kuwachinja shingoni kwa kutumia kisu.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mauaji hayo yalitokana na wivu wa mapenzi ambapo mume huyo alikuwa akimtuhumu mke wake kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu aliejulikana kwa jina moja la Hamza mkazi wa Kawe Dar es Salaam.

Taarifa hiyo ya Polisi imeeleza kuwa Mume huo wa Marehemu akiwa na rafiki yake alimlaghai mkewe waongozane pamoja wakiwa na mtoto wao kwenda kuangalia Ujenzi wa nyumba yao eneo la Kaole wilayani Bagamoyo lakini walipofika huko ndipo walipomchinja mke na mtoto.

Miili ya Marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya Bagamoyo na itakabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi.