Monday , 18th Apr , 2016

Tanzania bado inatarajia kupata mvua kubwa zaidi ambazo zitaendelea kunyesha kutokana na kuwepo kwa kimbunga kikali kiitwacho Kantala kinachovuma kwa kasi kubwa katika bahari ya Hindi.

Akizungumza na East Africa Television Mkurugenzi wa Uendeshaji Mifumo kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) Bi. Hellen Msemo amesema mvua kubwa zinatarajia kunyesha na kwa kiwango kikubwa zaidi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Mikoa ya Pwani sambamba na mikoa yote iliyopitiwa na bahari ya Hindi.

Amesema TMA wanaendelea kufuatilia kimbunga hicho ili kutoa tahadhari stahiki ambazo zinaweza kuchukuliwa kwa haraka ili kupunguza majanga zaidi yasiendelee kutokea sambamba na wananchi kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinavyoelekeza ili kujiepusha na maafa na kusisitiza wananchi kuacha tabia ya kupuuza tahadhari hizo.

Bi. Hellen amesema mafuriko na majanga yanayoendelea kutokea nchini yanachangiwa na kuwepo kwa miundombinu mibovu hali inayosababishwa na wananchi wenyewe hivyo amewataka wananchi kuacha kutupa taka ovyo ambazo zinaenda kuziba njia za kupitisha maji kwa haraka.

Amesema Mamlaka ya Hewa kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa wameanzisha mkakati wa kujikinga na majanga mbalimbali na wameanza kutembelea mikoani ambako wananchi wake hawapati taarifa kwa wakati kutoa vipeperushi maalum vyakuwasaidia wananchi katika kujua mwenendo wa hali ya hewa nchini.