Tuesday , 22nd Mar , 2016

Kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa stars kimekamilika baada ya kundi la pili la wachezaji waliosalia kutua mjini D’jamena ambao hali ya hewa ni joto kali tayari kwa mchezo dhidi ya wenyeji Chad utakaopigwa kesho alasiri kwa saa za Chad.

Stars waliotangulia wakijifua wakiwa na nahodha mpya wa timu hiyo Mbwana Samata kushoto.

Msafara wa mwisho wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Taifa stars umetua salama usalimini katika mji wa D’jamena nchini Chad ukiongozwa na mkuu wa msafara wa timu hiyo ambaye ni Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Ravia Idarus Faina na moja kwa moja kuungana na kikosi kilichotangulia kikiwa na benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha mkuu Boniface Mkwasa.

Kocha mkuu wa timu hiyo Boniface Mkwasa amesema anaimani na kikosi chake kesho kitafanya vema na kuwazima wenyeji ambao wameanza kuingiwa na mchecheto kuelekea mchezo huo ambao utapigwa kuanzia majira ya saa 9 alasiri, siku ya Jumatano sawa na saa 11 kwa saa za nyumbani Tanzania na Afrika Mashariki.

Mkwasa amesema kikosi kilichotangulia hakina majeruhi yeyote na jana kilifanya mazoezi kuanzia majira ya saa 9 alasiri, ikiwa ni sawa na muda utakaochezwa mchezo huo hapo kesho siku ya Jumatano sawa na saa 11 kwa saa za nyumbani Tanzania.

Aidha Mkwasa maesema mazingira ya mji wa D’jamena hali ya hewa ni joto kali tofauti na nyumbani, na kwa siku mbili walizofanya mazoezi, anaimani vijana wake wameweza kuzoea hali ya hewa na kufanya vizuri katika mchezo huo wa Jumatano.

Mkwasa amesema hana shaka na utimamu wa mwili wa wachezaji wake kwakuwa wachezaji wake wametoka katika vilabu vyao ambavyo vilikua na michezo mwishoni mwa wiki, hivyo ni wazi wote bado wako fit kikubwa ni kuhakikisha wanafanya maandalizi ya mwisho kwa ajili ya mchezo huo.

Amesema “Hatujapata muda mrefu wa kufanya mazoezi kwa pamoja, wachezaji walikua na majukumu katika vilabu vyao, nashukuru wote wamewasili wakiwa salama na waliowasili leo wataungana na wachezaji wenzao kwaajili ya mazoezi ya mwisho alasiri ya leo na pia mchezo wenyewe”.

Akimalizia Mkwasa amewaomba na kutowa wito kwa Wataznania wote kuiombea dua timu yetu ambayo kesho itashuka dimbani katika uwanja wa Omnisports Idriss Mahamat Ouya ulipo katika jiji la D’jamena Chad kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2017.