Mandhari katika eneo la biashara la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa uvumi huo, chanzo cha mgomo huo ni hatua ya wafanyabiashara kupinga ukaguzi unaofanywa na mamlaka ya mapato kwa kushirikiana na jeshi la polisi, wa kukagua wafanyabiashara wasiotoa risiti kwa bidhaa wanazoziuza.
Msemaji wa Jumuiya hiyo Bw. Steven Chamle ameiambia EATV kuwa biashara katika eneo la Kariakoo zimeendelea kama kawaida na kwamba kilichosababisha baadhi ya maduka kuchelewa kufunguliwa ni mkutano ambapo maofisa wa TRA walikutana na wafanyabiashara hao kwa lengo la kutoa ufafanuzi juu ya operesheni hiyo.
"Taarifa za mgomo sio za kweli bali kilichotokea ni mkutano ambapo idadi kubwa ya wamiliki na wauzaji wa maduka walihudhuria, mkutano ulioitishwa na Mamlaka ya Mapato mkoa wa Ilala kwa lengo la kutoa elimu juu ya zoezi linaloendelea la kuhakikisha wafanyabiashara wanatoa risiti," alisema Chamle.
Ameongeza kuwa zoezi hilo ni rasmi na linaungwa mkono na Jumuiya hiyo kwani kuna baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa sio watiifu kwa kutotoa risiti kwa mauzo wanayoyafanya.
Ameongeza "Sheria ya matumizi ya mashine za EFD inahusisha wafanyabiashara laki mbili tu kati ya takribani wafanyabiashara zaidi ya milioni mbili waliopo nchini hivi sasa na kwamba risiti za kuandika kwa mkono bado zinatumika kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao hawapo kwenye mfumo wa mashine za EFD,"
Aidha, msemaji huyo wa jumuiya ya wafanyabiashara amesema wao kama jumuiya wanaunga mkono operesheni hiyo na kamwe hawapo tayari kutetea wafanyabiashara wasiotoa risiti kwani kitendo hicho kinalenga kuinyima serikali mapato na hivyo kukwamisha shughuli za maendeleo.