Monday , 14th Mar , 2016

Bondia Mtanzania kutoka Tanga ambaye ni mahiri wa kurusha makonde mazito Said Mbelwa ametamba kumsambaratisha mpinzani wake katika mpambano wao wakuwania mkanda wa PST ambao anaushikilia kwa sasa akiutetea dhidi ya Ibrahim Tamba wa Dar es Salaam.

Bondia Said Mbelwa akijifua kujiandaa na mpambano wake dhidi ya Ibrahim Tamba.

Bondia wa kimataifa wa ngumi za kulipwa nchini Mtanzania Said Mbelwa kutoka Tanga anataraji kutetea mkanda wake wa ubingwa wa kimataifa wa PST kwakuvaana na bondia Chipukizi mwenye kipaji Ibrahim Tamba katika mpambano wa raundi 12 uzito wa juu utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu jijini Dar es Salaam.

Wakiongea hii leo katika kambi ya mazoezi ya bondia huyo katibu mkuu wa PST Antony Ruta amesema maandalizi yamekamilika huku Mbelwa na kocha wake Michael Mwakenja wakitamba kuibuka na ushindi na kutetea mkanda huo.

Tamba ambaye anauzoefu wa hali ya juu amekuwa katika mazoezi ya muda mrefu sasa akijiwinda na mpambano huo ambao yeye ametamka wazi kuwa hali hiyo imetokana na kuupa kipaumbele kikubwa mpambano huo ambao unataraji kuwa mgumu mno hasa kutokana na uwezo na kipaji cha hali ya juu alichonacho mpinzani wake huyo.

Aidha Mbelwa amesema pamoja na uchanga wa mpinzani wake lakini kamwe hiyo haitakuwa sababu ya yeye kumdharau ama kumchukulia kwa kawaida mpinzani wake hivyo yeye anamchukulia kwake ni mshindani mkubwa ambaye naye anataka mkanda huo na ndiyo maana anafanya maandalizi ya kutosha kumdhibiti bondia huyo.

Tamba amesema anachokitazama kwa sasa ni kuhakikisha anajiweka sawa kwa mpambano huo na kwa hali ilivyo anajiamini kwa asilimia mia moja kuwa atamdondoshea kipigo kizito Tamba kama alivyofanya kwa mabondia wengine waliokutana naye wakiwemo kina Japhet Kaseba na Karama Nyirawila ambao walishindwa kufua dafu kwa mgosi huyo toka jijini Tanga.